ASANTE YA PUNDA NI MATEKE

Baba hata mimi nimeliwazia jambo hili kwa muda. Hata hivyo, moyo wangu umekuwa yabisi. Hisia zangu zimekufa ganzi na nimebaki na utulivu mdogo sana lau ningekuwa mwehu. Baada ya yote umewatendea, ni vipi wangekupiga kalamu bila utu hivi? Nilijiuliza huku nikiwa nimelala chali sakafuni.

Mawazo mazito yalikumba akili yangu na kunipagaza na kimuyemuye usiokuwa na kifani. Nilishindwa ni vipi ambavyo nitaweza kutimiza azma yangu ya kuwa rubani? Je, kaka yangu mdogo hata ataweza kupata elimu ya msingi? Mama ataweza kutuandalia vyakula vitamu bado? Haya tu ni sampuli ya mawazo mengi yaliyoniteka nyara.

Nilihisi kichwa changu kikiwa moto, nilijikokota hadi kwenye bafu ili ninawe uso. Lo! Hamkuwa na hata tone la maji humo. Mlikuwa mmekauka mithili ya mfupa jangani. Nilikata kauli kuelekea mtoni kunawa uso. Nilipokuwa nikivaa viatu, nilimwona mama amejifunga kibwebwe katika maombi akiwa amepiga magoti na machozi kumtiririka njia mbilimbili.

Pia mimi nilipiga dua kabla ya kuelekea langoni. Hata wakati upepo mkavu ulipokuwa ukinipiga nilipotembea, haukubeba mawazo hayo nayo. Nilijizatiti kutabasamu lakini sikuwa na nguvu hiyo. Hatimaye baada ya kutembea nikiangalia ardhi, nilifika mtoni na kunawa uso.

Mtoni nilijiona na kuiona miti na ndege waliokuwa angani. Hayo yalinifanya nikumbuke siku hiyo abu alikuja na kutuambia habari hiyo ya kusikitisha. Ilikuwa jioni moja Alhamisi ambamo baba aliandamwa na waja wawili huku akiwa amevaa shati na kaptura pekee ilhali alienda na suti asubuhi.

Walimrusha kwa madaha ndani ya nyumba yetu na kumwambia, "hamna kazi ya kufanya tena". Hawakujali kama mimi na mama bado tulikuwa hapo. Baba alionekana amejawa na soni. Sote tulinyamaza kimya huku tukiangaliana kwa macho ya mshangao.

Baba alikuwa mwekahazina wa kampuni hiyo. Alifanya kazi hiyo humo kwa miaka saba, huu ungekuwa wa nane. Licha ya kuwa huko miaka hiyo yote na kuwa na utendakazi wema, hawakuwahi kumpandisha cheo. Lakini abu hakujali, alishinda kusema kuwa bora tuna ya kutosha ya kushughulikia mahitaji yetu, hamna wasiwasi.

Mimi na mama tuliamini na kukubali usemi wake. Licha ya kazi yake kama mwekahazina humo, alijipata akiwa dobi humo pia hususan kaka yangu mdogo Tole alipozaliwa. Nimepata fursa ya kutembelea humo ofisini na yakini tangu awe chura humo, vyoo vimekuwa safi dawamu.

Kwa kweli baba yangu alikuwa mja mwenye bidii na utendakazi kuu hivyo basi tuliachwa na vinywa wazi tulipojua amefutwa kazi. Baba yangu ndiye aliyetoboa kimya, na kutuambia, "Chuma na madini ndiyo imechukua kazi yangu, mimi ni gharama kwa kampuni ukinilinganisha na tarakilishi" huku akitokwa na machozi pande mbili.

Mimi na mama tulimkumbatia tukilia huku Tole akituangalia na macho makubwa. Kwa kweli asante ya punda ni mateke.