DUA LA KUKU HALIMPATI MWEWE

Owino alikuwa mkata katika mtaa wa Matamauko. Mtaa uliojulikana kote kwa vyumba vyake duni vya tope na nyasi. Mtaa wote ulinuka fe! Usiki kutwa na mchana kucha kwa kuwa wakazi wengi hawakuwahi tambua choo kama shimo maalum, sembuse utumizi wa mapipa.

Vyumba hivyo vilibanana kama ndizi na aghalabu majirani wangeweza kujua ni hamsini gani zilizoendelea katika vyumba vya wengine. Owino alitambua haya vyema, na hajawahi nunua redio wala runinga lakini kila jumamosi aliketi kwake na kufuatilia mechi za kusisimua ana kwa ana.

Katika mtaa huu, waja walitambuana vyema. Walikuwa na utangamano wa unapojikwaa, jirani huhisi uchungu. Hivyo basi mienendo ya kila mja ilijulikana, na hakuna aliyekana kuwa Owino alikuwa mja mwenye bidii za mchwa ajengaye kichuguu kwa mate.

Mchana alifanya vibarua vya hapa na pale vya kijungujiko. Si kupalilia mimea, si kuchuma minazi, si kujenga vyumba vidogo, mikono ya Owino iliona yote na nyayo zake zilichuana na ardhi kila siku na siku ayami kwa wasaa ndefu.

Je usiku? Usingizi ulimkwepa kama mwenye mafua. Wakatengana kama mbingu na ardhi. Kazi zake hazikutamatika mchana. Jua lilipotua, Owino alivalia shati ya samawati, sweta nyeusi na suruali kijani kibichi, na kujihami kwa kurunzi yake na hatimaye alielekea kufanya kazi yake maalum kutoka Jumatatu hadi Ijumaa.

Kampuni ya Lala Salama ndiyo ilikuwa mwajiri wa Owino. Kwa mwezi huu, alikuwa amechaguliwa kulinda jumba kuu la shirika la zaraa. Owino amekuwa kote, kutoka benki hadi hospitali hata majumba ya wakwasi. Yakini alikuwa na tajriba kemkem.

Owino aling'oa nanga saa mbili usiku akiwa amebeba rungu yake halisi ya kukabiliana na vinyangarika wowote. Kila siku hakuwacha kushangazwa na tofauti kati ya mtaa wake na mitaa alikokwenda kulinda. Mandhari yalibadilika kwelikweli.

Kutoka kwa mtaa wa baiskeli na kuingia katika mtaa wa mashangingi yenye baraste na huko kwao ni vichochoro tu. Usafi nao je? Hakukuwa na hata chembe ya taka. Kwa kweli alishinda kutamani maisha kama haya ya hewa safi na baraste kuu, ndio maana alijikaza kibwebwe kazini.

Owino daima dawamu hakuchelewa kazini na hakupatwa na hata lepe la usingizi. Ndio maana waajiri wake walimpa kazi katika sehemu kuu ilhali mshahara wake ulibakia vivyo hivyo wa kijungujiko. Hata masurufu hakuwahi pewa hata kama pahali pa kulinda palikuwa mbali sana.

Hakupenda haya, hivyo basi aliendelea kufanya bidii zaidi kwa kuwasili mapema zaidi na kukuja kulinda hata siku ambazo hakuwa na zamu. Isitoshe, alijipata mara kwa mara akichuana na majangili na kila mara aliweza kuwakimbiza mbali pasi na yeye kujeruhiwa kila mara.

Alikuwa na matumaini kuu ya kuongezwa mshahara na hakuwahi chushwa na kuwatumia nyaraka. Nyaraka ambazo zilirejeshwa kila mara bila jibu. Haya kweli yalikuwa ya kutamausha lakini Owino alihimili haya yote kwa kuwa hakujua kwengine angetorokea. Yakini dua la kuku halimpati mwewe.