KIMUYEMUYE
Nilipotazama Gazeti la Tangaza Leo, anwani ilinikodelea macho: Shule nyingi zakosa matokeo ya mtihani wa kitaifa wa KCSE. Nilikodoa huku nikiachama na baridi shadidi ikiwa imevamia jasadi yangu. Mawazo kemkemu yalinizunguka akilini huku nikiwa nawaza na kuwazua kuhusu mustakabali. Kwa nini mwaka huu? Shule zipi? Kina nani? Maswali ya sampuli hii yalivuruga utulivu wa moyo wangu. Nao moyo ulianza kututa.
Nilisimama tisti na kupumua polepole kwa kuwa sikutaka kuongeza shinikizo la damu. Haikuwa habari rahisi ya kupokea. Afadhali ningetumia shilingi hizo hamsini kununua mkate asubuhi hiyo. Kusoma anwani hiyo ilikuwa kama kumeza kiazi kitamu bila kinywaji.
Nilikumbuka kuwa kifo cha wengi ni harusi na hivyo basi nilijiandaa kuenda kusambaza habari kwa majirani. Nao pia walishika tama na wengine walibung'aa huku wakiniuliza maswali yayo hayo nisiyokuwa na majibu yao. Machozi yalianza kutiririka kwenye wajihi wa wengine. Wengine nao walitafuta la kunifyatulia, niliwakumbusha kuwa mimi ni msambazaji habari tu, si munda habari.
Nilirudi nyumbani nikiwaza ni vipi mwana wangu ataipokea habari hii. Yeye ndiye aliyekuwa kifungua na kifunga mimba wangu. Ni yeye aliyekuwa ameufanya mtihani huo. Jua lilikuwa likimaga akiwa vitabuni na bado lilimpata akijishughulisha na usomi wake. Kwa kweli, alitia juhudi za mchwa ajengaye kichuguu kwa mate. Sasa kiwewe cha mtego wa panya ambao huingia waliomo na wasiokuwamo kilipiga hodi.
Je, huu ndio mwisho wa azma yake ya kuwa daktari? Chanda chema hautavishwa pete? Jitihada haitalipa walimwengu? Haya ndiyo maswali yaliyonitia kimuyemuye. Hata nguvu ya kunyonga baiskeli yangu ilianza kupungua karibu initoroke.
Hatimye niliwasili nyumbani na kuketi kwa tako moja nikiwazia ni vipi nitamwambia haya. "Do! Do! Do!" mbisho ulisikika mlangoni. Hakukuwa na hata tembe la shaka, nilijua ni mwanangu. Jasho jembamba lilitiririka mgongoni mwangu na magoti yangu yalianza kuchezacheza lakini baada ya kujikakamua niliweza kusimama.
Nilipokuwa nikitembea asteaste hadi kwa mlango, nilikumbuka shubiri iliyonibidi nimeze ili niweze kumwelimisha. Vibarua kadhaa vya kijungujiko ndivyo vilivyokuwa karo yake. Licha ya kufanya kazi ya kupinda mgongo huku jua likikufokea kwelikweli, waajiri nao walikuwa wapyaro wasiokuwa na utu. Matusi na masimango ndiyo waliyokuwa wakibadilishana kunihusu kila siku. Walisahau la wahenga kuwa aliyewapa kiti ndiye aliyenipa kumbi.
Licha ya hayo niliendelea kujizatiti kwa kuwa lislo budi hutendwa na hatimaye haba na haba hujaza kibaba. "Hujambo!" nilimsalimu mwana, sidhani hata alinisikia, alitembea moja kwa moja na kulichukua gazeti tu. Alipindua ukurasa na kuendelea kusoma kwa kina kisha akatabasamu.
"Alhamdulilahi! Shule yetu haipo miongoni yao" alisema kwa furaha. Utulivi wangu ulirejea nilipoangalia orodha ya shule mia moja na hamsini iliyokuwa kwenye ukurasa wa pili. Sasa niliweza kuketi kwa makalio yote mawili, nilimshukuru Mola kwa kupiga dua na kujipa ahadi kuwa sitawahi kukimbilia wasiwasi kabla ya kuelewa jambo fika.