KINOLEWACHO HUPATA

Paukwa! Pakawa! Palikuwa na kitongoji mahususi kilichoitwa Nishati. Kitongoji hiki kilikuwa katika taifa kuu la Vushati. Kilikuwa kitongoji cha kawaida kwa wengi na kwa miaka ayami. Kilikuwa na waja wake waliojizatiti kufanya shughuli zao kemkemu za kila siku.

Walimu, maseremala, wakulima na hata wavuvi walipatikana humu. Kweli ilikuwa kitongoji cha kawaida kama vitongoji vingine, lakini hayo ni ya jadi. Hali ya kijiji hiki kilibadilika na kupata umaarufu maalum kwa sababu ya kisa ya ghulamu mmoja. Ghulamu aliyezaliwa na kukua na hata kubugia chumvi humo Nishati. Ghulamu huyu aliitwa Rangi.

Inasemekana kuwa siku ambayo Rangi alizaliwa, nyota ya jaha ilionekana tena angani. Wakunga hawangeweza kusitiri tabasamu zao wazi walipomwona. Alikuwa mtoto mwenye ucheshi na utulivu mwingi, utulivu ambao ungewaondoa ibilisi wowote kokote.

Rangi alilelewa kwa tunu na tamasha. Aushi yake ilikuwa ya asali kwa maziwa. Hakuwahi kosa mavazi ya kung'ara wala kitanda cha foronya, sembuse chakula cha kutia kinywani. Haya ndiyo yaliyokuwa maisha ya Rangi.

Yalikuwa hivyo hadi alipokuwa na umri wa miaka kumi na minne. Maisha yake yalichukua mkondo mpya. Mkondo ambao ulijaa vizingiti tupu. Jumamosi moja, Rangi aliamshwa kwa kemi za nina yake. Aliona miili mikubwa yenye misuli tinginya ikinasa wavyele wake. Rangi alifyatuka kama mshale ili awasaidie lakini muda ulishakuwa umeyoyoma maadamu hakuwaona wavyele wake pahali popote.

Hayo yalimsikitisha Rangi, lakini miili hiyo ilitaka bado kuongezea chumvi kwenye kidonda, hivyo basi ilimwambia Rangi aponye miguu na asiwahi kanyaga humo tena. Kwa hofu Rangi aliponyoka. Hakujua pa kuenda lakini miguu yake haikusita kumbeba. Huu ndio ulikuwa asili ya balaa na matatizo ya Rangi.

Afya yake ilidhoofika pakubwa. Ilimbidi ale kutoka mapipani chakula kilichovunda na kuvundiana. Yeye pia alianza kunuka kama chakula hicho kwa kukosa maji ya kuoga. Hii ndiyo ilikuwa hali yake kwa miezi. Hatimaye alichushwa.

Alichushwa kweli. Alikata kauli kuwa maisha haya hayafai, alijizatiti na kung'oa nanga kurudi nyumbani ili akabiliane na miili hiyo. Alipofika, hata kabla ya kunyoosha miguu, alijipata amepeperushwa angani na mmoja mwenye misuli tinginya. Ilimbidi afanye miguu impone tena.

Aliona kuwa dawa la moto ni moto, hivyo basi naye pia aligundua anahitaji miraba minne pia. Rangi hakupoteza wakati, alitia bidii za mchwa katika mazoezi na hata alianza kuvua na kuwala samaki. Baada ya mwezi, aliweza kusimama kwa mikono yake kwa dakika tano. Rangi alijitanua kifua na kuelekea nyumbani tena.

Alipochuana nao tena, aliweza kumbwaga mmoja chini lakini hao wengine wawili walimvamia na kumpeperusha nje lakini mara hii hakupeperushwa mbali sana kama wakati uliopita. Hivyo basi Rangi aliendelea na mazoezi yake ya nguvu. Hata alianza kufanya vibarua kadhaa zinazohitaji bidii nyingi.

Hata kama malipo yalikuwa ya kijungujiko, haba na haba hujaza kibaba, aliweza kujinunulia vyakula vya kushibisha sasa. Baada ya miezi miwili, alirudi. Aliwakusanya wote watatu kama magunia na kuwapeperusha nje ya jumba lake. Kutoka siku hiyo hawajawahi onekana tena humo. Baadaye hata wavyele wake walirudi waliposikia kuhusu ushujaa wa mwana wao. Yakini kinolewacho hupata.