KISA CHA KUSIKITISHA

Nilimtazama kwa muda. Moyo wangu ulinituma kumwuliza kilichomfanya kuishi katika mazingira ya kudhalilisha kama haya lakini nilikataa katakata kuwa mtumwa wa roho yangu katika suala hili maadamu ni mwehu pekee anayejadiliana na jogoo.

Mangisi huyu alikuwa amelala topeni chini ya mwembe labda kwa kukosa chakula. Baadhi ya manyoya yake yalikuwa yamefifia, alionekana amekonda na kukondeana mithili ya muwa. Nilishindwa ni kwa nini hangevuka mipaka ya konde hilo la tope na kuenda kuchakura kama wenzake. Kisha nikakumbuka kuwa hata binadamu anahitaji chakula ili apate nishati.

Jogoo huyu alikuwa amehuzunika kweli, baada ya ukame wa kuliza kumpokonya mke wake na vifaranga wake, hajawahi wika vile ambavyo alikuwa akifanya kila kuchao, ni kama simanzi ilitia gundi kwenye kidomo chake. Yakini ungemwona jimbi huyu, ungehuzunika pia.

Mzee Tatizo ndiye aliyekuwa mmiliki wa kishingo huyu. Alikuwa akimlisha vyema kabla ya ukame kudhuluma mihindi yake shambani. Aliwachwa bila chakula chochote wala bidhaa zozote za kuuza. Isitoshe ukame huu ulimfanya kitindamimba wake kuenda jongomeo, hali hii iliwasikitisha sana.

Mzee huyu mwenye hekima alijikakamua kutia bidii ili aweze kukimu mahitaji ya familia yake. Alianza kufanya vibarua vya kijungujiko ili aweze kufikisha mkono mdomoni, alielewa fika kuwa mgaagaa na upwa hali wali mkavu. Hivyo basi aliweza kuhakikisha aila yake haingelala njaa wiki nzima.

Katika hali hii ya masikitisho, ilikuwa nadra sana kupata Tatizo akimlisha jogoo wake maadamu mja hujikuna ajipatapo. Hangeweza kukimu mahitaji ya aila yake na jogoo wake kila wakati. Hivyo basi alipea aila yake kipaumbele vile ambavyo baba yeyote mwema angefanya.

Wandani wa mzee huyu walimrai kumwuza jimbi wake ili aweze kupata hela za kumkimu lakini maombi yao yaliangukia masikio yaliyotiwa nta. Je, ni baba yupi aliye na akili timamau ambaye angeweza kuuza zawadi aliyopewa na kitindamimba wake kabla aage dunia? Yakini mzee huyu alisononeka sana kumwona jogoo wake akiteseka hivi. Alihisi kana kwamba anamkosea kitindamimba wake sana.

Kivuli cha mwembe alichopenda mangisi huyu hata hakikuwa cha mzee Tatizo, kilikuwa cha jirani wake Tunda aliyependa sana kupanda matunda. Aghalabu Tunda angempa mzee Tatizo matunda kadhaa ya kujikimu hata kama hayakuwa mengi baada ya ukame. Kitendo hiki cha kidugu kilimfanya Tatizo kuamini ya wahenga kuwa jirani ni ndugu.

Ilikuwa Jumapili, aila ya mzee Tatizo ilikuwa inarejea nyumbani baada ya misa ya kufana. Tatizo alirejea nyumbani na nafaka chache za kumlisha jogoo wake, lo! Ilikuwa afadhali apike na ale nafaka hizo maadamu Mola alishamchukua kiumbe wake usiku uliopita. Aila hiyo ilisononeka sana, milio ilisheheni nyumbani humo huku machozi yakitiririka kote. Mangisi huyu alizikwa pale pale ambapo kitindamimba wake alipozikwa.