SULUHISHO ZA TATIZO LA MIHADARATI

Janga hili limeenea kuenea. Si kwa vijana wa mijini tu bali pia kwa vijana wa mashambani pia, hakuna aliyesazwa. Ndumakuwili huyu lazima auliwe na azikwe katika kaburi la sahau awache kutupa kimuyemuye kila kuchao. Hivyo basi ningependa kuwajuza kuhusu silaha ninazoona mwafaka za kuchuana na hasimu huyu.

Kwanza, ni vyema kuamini ya wahenga kuwa elimu ni taa, gizani huzagaa. Vijana wengi katika umri wao mdogo hawafahamu fika madhara ya adui huyu. Wamepumbazwa na uongo mwingi unaotoka kwa waja wasiojua bee wala tee kuhusu janga hili. Vijana wetu wanapaswa kujua ukweli wa mambo ili wasianguke katika shimo hili kiholela.

Askari wetu nao wanapaswa kujikaza kisabuni zaidi ili kuwasitisha wananowalaghai vijana wetu na kuwauzia liga hili. Wanapofanya hivi, wengi watachelea na kuwaza mara nne kuhusu thamani ya aushi yao kabla ya kujihusisha na biashara hii mbovu.

Ingekuwa vyema kwa vijana kuwa na njia mwafaka ya kutangamana, hususan katika michezo. Hivi watakuwa na jambo bora la kujishughulisha nalo na kuweza kuepuka shughuli haramu kama utumizi wa dawa za kulevya

Vijana nao waajibike wanapowachagua waja wa kujihusisha nao. Shinikizo la rika ni tatizo la kweli hususan baina ya vijana. Aghalabu utapata ni mja mmoja tu anayejitumbuiza katika utumizi huu kisha wengine wanamfuata. Haya yanaonyesha ukweli wa methali inayosema: "samaki mmoja akioza ni mtungo pia."

Nao kwa kuwa vijana hawana hekima inayomithilika na ya waveyele wao, ni vyema waveyele wao wajishughulishe na hamsini za watoto wao. Na si wazazi tu, mtoto ni wa jamii! Hivyo basi sote tuna hilo wajibu la kuwatunza na kuwaelekeza.

Nafasi za ajira nazo zinapaswa kuongezeka, ili vijana wanapofuzu chuo kikuu wasife moyo huku wakibisha kwenye milango iliyofungwa kitambo sana. Katika hali hii ya kukosa matumaini, ni rahisi sana wajitumbuize katika mihadarati huku wakijaribu kujiliwaza.

Vituo vya kurekebisha uraibu navyo vipewe kipaumbele vinavyostahili. Hivi, vijana wetu waliozamia zii katika dimbwi hili linaloangamiza watapata msaada ufaao kutoka kwa waja wanaoelewa mambo haya fika. Na hata wao baada ya kusaidiwa wataweza kuwasaidia wanaopitia waliyopitia.

Hatimaye, ushauri nasaha unapaswa kutolewa kwa vijana wetu, hususan wa ana kwa ana. Hivi uchungu walio nao utaweza kububujika na mioyo yao yataweza kutulia. Hawatakuwa na sababu yoyote ya kujitumbuiza katika shughuli haramu kama utumizi wa mihadarati maadamu watakuwa na sahibu mwengine wa kuamini, si ndumakuwili huyu.