Mwandishi Bora,
Sanduku la Posta 35-453,
Mombasa.

Januari 9, 2022.

Waziri wa Usalama wa Ndani,
Sanduku la Posta 37-875,
Nairobi.

Kwa Mheshimiwa,

KUH: UDUMISHI WA AMANI
Nina furaha kemkemu kwa kuwa na fursa hii halisi ya kukuandikia waraka huu. Sote tunafahamu fika kuwa wakati nyeti unatujongelea. Majira ya kuwachagua watakaotuongoza kwa miaka mitano ifuatayo. Hivyo basi, bila kupoteza wakati, ningependa kupendekeza namna za kudumisha amani wakati huu.

Kwanza, umma unapaswa kuelimishwa. Wenye hekima hawakutulaghai waliponena kuwa, "elimu ni taa, gizani huzagaa." Waja wanafaa kufahamu dhahiri shahiri kuwa jirani yake hageuki kuwa adui wakati huu. Kwa jirani yake kumchagua mwanasiasa tofauti haimfanyi awe adui. Inamaanisha tu kuwa ana maoni tofauti na wewe. Ujumbe huu unapaswa kuenezwa kote na watu wanapaswa kuheshimu maoni ya wengine kwa kuwa heshima si utumwa.

Pili, idadi ya polisi inapaswa kuongezwa. Isitoshe, malipo yao yaongezeke pia ili wasifanye kazi yao shingo upande. Polisi wanapowekwa katika kila pembe ya nchi, waliokuwa na nia za ugomvi watachelea. Wachonganishi watawaza na kuwazua kama wangependa kutiwa mbaroni mapema hivi.

Vilevile, wanasiasa wanapaswa kupewa nasaha ili wawajibike. Maneno yao hayafai kuwafumukanisha waja ila yanafaa kuwajumuisha. Wasithubutu kuwasimanga wanasiasa wapinzani maadamu katika umati uo huo utawapata wafuasi wa wapinzani. Haya aghalabu husababisha ugomvi mtupu na waja huumia. Wanapaswa kukumbuka kuwa ulimi ni upanga.

Isitoshe, walioathiriwa na ugomvi wa uchaguzi uliopita wanapaswa kushughulika ila kuna uwezekano watalipiza kisasi. Katika uchaguzi fulani, ugomvi ulikuwa mwingi sana. Wengi walipoteza aushi zao na wengine zaidi waliachwa na upweke sembuse machozi. Hali hii ya huzuni aghalabu hugeuka na kuwa maya na humfanya mja apoteze akili yake razini. Kupunguza visa kama hivi, waja hawa wanapaswa kupewa usaidizi utaowafaa.

Aidha, saa za kutoka nje zinapaswa kudhibitiwa. Si siri kwa yeyote kuwa usiku ni libasi bora. Hivyo basi huwa wakati mwafaka kwa wakora kutekeleza uovu wao. Kuchuana na haya, saa za waja kuwa nje zinapaswa kupunguzwa hadi wakati ambapo jua litatua. Kwa kuwa lisilo budi hutendwa, itawabidi wakora hawa kufanya hamsini zao mchana, nao polisi wetu watawaona bila tatizo na kuwanasa hapo hapo.

Licha ya hayo, utangamano na viongozi wa dini utasaidia. Viongozi hawa wataweza kuyainua mioyo ya waja wanapowahubiria kuhusu umuhimu wa amani. Watawafunza kuwapenda majirani wao, na je, ungependa kumwumiza unayempenda? Vilevile maombi yao na ya wote wenye imani yatasaidia kwa sababu Mungu haachi mjawe.

Pia, takwimu za kura zinapasswa kuthibitishwa. Kuna msemo unaonenwa hivi, "kura yako si hoja ni wanaoihesabu ambao ni hoja." Haya ni kweli. Hauwezi kumfanya mwewe hakimu katika kesi ya kuku. Hivyo basi, wote wanaohusika na shighuli hii wanapaswa kukaguliwa kwa makini na kazi yao pia kukaguliwa vivyo hivyo.

Mwisho, utangamano na jumuiya ya kimataifa ya kudumisha amani unafaa. Kwa kufanya hivi tutaweza kupata usaidizi tunaouhitaji na hata kuimarisha maarifa yetu kuhusu suala hili nyeti. Tukumbuke kuwa jifya moja haliinjiki chungu.

Kwa hayo machache ningependa kutia kitone cha mwisho cha waraka huu. Asante sana kwa kuusoma na natumai kuwa utayatilia maanani mapendekezo haya. Kwa kufanya hivi, bila shaka lolote, tutakuwa na kipindi cha uchaguzi chenye amani ghaya.

Wako mwaminifu,

Signature

Mwandishi Bora.